Naitazama bahari, kama mpenzi aliyopotea,
Miguu yangu juu ya mchanga, joto lake tanuru
Pole pole naisogelea, macho yangu yaitazama,
Na kamwe hayapepeseki
Bahari uja nakuondoka, unionea aibu,
Bahari uja nakuondoka, unidadisi,
Kisha yanipa mabusu miguuni
“Karibu” “karibu” huninong’oneza
Kwa pepo tulivu za mashariki
Maji uzidi kunivuta, mwili wangu waanza kuzama,
Unyayoni, magotini, Kifuani na kichwani
Namezwa tumboni kwake, ambalo kamwe hushibishwi
Naanza pambana, miguu yarusha mateke,
Mikono vibao, naishiwa pumzi, naishiwa nguvu
Sauti ya utulivu ikanijia
Tulia, achilia, tulia achilia
Bila njia nyingine na kwakuchoka kwangu
Naamini, natulia, naachilia
Naachilia majonzi ndani ya moyo wangu
Naachilia watu niliowafunga kifuani kwangu
Naachilia mitazamoya akili yangu
Naachilia matarajioyangu
Natulia, Naachilia
Ghafla mwili ukavaa wepesi, nikaanzaelea
Bahari ndani ya masikio yangu, jua likinipapasa ngozi yangu
Macho yakiwa yamefungwa, bahari ikageuka mbingu
Nikajazwa na furaha, amani isiyo simulika
Muda ukasimama, napale nikatamani kubaki milele
Hapo nikapata ufunuo, haikuwa bahari yenye tatizo
Bali ni mimi mwenyewe, nilitaka kuuwa nafsi yangu.