Bismillahi naanza, kwa jina lake manani,
Hakika yeye wa kwanza, alotuletea dini,
Adam alimfunza, apokuja duniani,
Ramadhani twafuturu, kwa pamoja uwanjani.

Dini imetuhimiza, tuwepo msikitini,
Sote tuwe tunaweza, kuwa pamoja jamani,
Hilo tunalitimiza, bila ya shaka yakini,
Ramadhani twafuturu, kwa pamoja uwanjani.

Uzuri wa mila zetu, tunafanana na dini,
hatuwachi mila zetu, tukafata za ugeni,
toka enzi babu zetu, walokuwa vijijini,
Ramadhani twafuturu, kwa pamoja uwanjani.

Twaweka chakula chetu, hapo nje uwanjani,
Tunakula na wenzetu, kwa pamoja mkekani,
Kwenye masinia yetu, wala sio sahanini,
Ramadhani twafuturu, kwa pamoja uwanjani.

Anayepita njiani, wakati wa kufuturu,
Akaribishwa jamvini, aketi na kufuturu,
Huo wema kwa mgeni, naye huwa ashukuru,
Ramadhani twafuturu, kwa pamoja uwanjani.

Watu huwa furahani, wanapokuwa pamoja,
Vicheko vimdomoni, wala huulizwi hoja,
Pamoja na majirani, wote wawezao kuja,
Ramadhani twafuturu, kwa pamoja uwanjani.

Tudumishe mila zetu, tusiache abadani,
Tuthamini yalo yetu,  tusifate ya wageni,
Ndio umuhimu kwetu, tuyapende kwa moyoni,
Ramadhani twafuturu, kwa pamoja uwanjani.

Part of SAWTI Zine Issue 1

Illustration by Mosab Zkaria

SABRA ALI AMRANI
SABRA ALI AMRANIPOET
Sabra Ali Amran, nimezaliwa Zanzibar. Nimesoma katika shule za msingi Mtendeni na Msasani. Shule ya sekondari ya Forodhani zote zilizopo Dar es salam. Ninamiliki stashahada ya juu ya uhasibu (Advanced Diploma in Accountancy) niliyoipata Chuo cha cha usimamizi wa fedha (IFM).Kilichopo Dar es salaam. Pia ninamiliki C.P.A-I (T) (Certificate Public Accountancy ) ya Bodi ya Taifa ya wakurugenzi na wahasibu (NBBA). Kipaji changu ni uigizaji wa filamu,utunzi wa hadithi na mashairi. Nimeigiza filamu : Kisasi cha Utata, Eda, Ramadhani Kareem, Boxera na Kaundime. Nimetunga vitabu vya hadithi: Sikitiko na Tabasamu la Huba.