
Illustration by Mosab Zkaria
Moyo hupenda kizuri, na pia chenye thamani,
Na hata uwe jabari, huingia mtegoni,
Utapenda cha fahari, kinachogusa moyoni,
Taarab za zamani, muziki ulo laini,
Sauti za waimbaji, ni nzuri ziso kifani,
Mungu kawapa kipaji, usiulize kwa nini,
Na tuwavishe mataji, yalo mazuri kichwani,
Taarab za zamani, muziki ulo laini,
Tusitupe mila zetu, tukafata za wageni,
Hiyo ni hazina yetu, na yenye kubwa thamani,
Kutoka mababu zetu, walitwachia zamani,
Taarab za zamani, muziki ulo laini,
Huimba kwa taratibu, wakiwepo jukwaani,
Hakika huoni tabu, kusikiliza yakini,
Masuali na jawabu, hupatikana nyimboni,
Taarab za zamani, muziki ulo laini,
Hizi ni nyimbo asili, ya wetu utamaduni,
Tusiitupe asili, tukaiwacha jaani,
Tupende na kukubali, mila zetu za zamani,
Taarab za zamani, muziki ulo laini,
Muziki wenye kanuni, umejaa ubunifu,
Vyombo hivyo vya zamani, vilipigwa bila khofu,
Na ukiwa jukwaani, hausikii uchofu,
Taarab za zamani, muziki ulo laini,
Taarabu ina raha, unaihisi moyoni,
Ikiwa moyo wahaha, utapata burudani,
Tulia upate raha, unapokuwa nyumbani,
Taarab za zamani, muziki ulo laini,